Mapigano yameripotiwa kuongezeka nchini Yemen kati ya wanajeshi wa serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa na Wahouthi, jeshi la serikali ya Yemen likidai kuwauwa wapiganaji 190 wa Houthi.
Jeshi la serikali ya Yemen limedai pia kuharibu mamia ya makombora ya Wahouthi kwenye makabiliano kati ya pande hizo mbili.
Majed Abdullah al-Nuzaili, Msemaji wa wanajeshi wa serikali ya Yemen, amesema mashambulio yao yalilenga ngome za Wahouthi katika maeneo ya Lahij, Taiz, Marib, al-Jawf, Hajjah na al-Bayda.
Katika taarifa yake, Majed amesema jeshi la Yemen lilitekeleza karibia mashambulio 29 ya angani na kurusha droni 39.
Aidha ameeleza kuwa walirusha makombora 62 na mashambulio mengine 744 dhidi ya ngome hizo za Wahouthi.
Mapigano nchini Yemen yanajiri wakati huu kukiwa na wasiwasi ya kurejea tena kwa vita vya Iran, Marekani na Israeli mashariki ya kati.
Serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa na kuungwa mkono na Saudi Arabia, imeanzisha mashambulio yenye lengo la kuchukua maeneo yanayokaliwa na wapiganaji wa Houthi tangu mwezi Septemba.
Wahouthi kwa upande wao wamekuwa wakiteleza mashambulio dhidi ya Saudi haswa katika viwanja vyake vya ndege na viwanda vya mafuta, Wahouthi wakisema wanachukua hatua hiyo kujibu mashambulio ya Saudi dhidi yao.