Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema hataki kuona migogoro ya kugombea madaraka ikiendelea kujitokeza katika taasisi zilizo chini yake, kwa kuwa zinavuruga na kuathiri ustawi wa watumishi kutoa huduma.
Mbali na migogoro hiyo, amesema pia tatizo la msongo wa mawazo, hasa kwa waajiriwa wapya, linawatesa kwa sasa, hivyo linapaswa kutafutiwa mwarobaini wa kudumu.
Waziri Sangu, ameonya hayo jana (Novemba 11,2026) jijini Arusha, wakati alipokuwa akizungumza na waajiri kutoka sekta ya umma na binafsi, na viongozi wa matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE.
"Serikali imepokea malalamiko kuhusu baadhi ya waajiri kutotambua umuhimu wa vyama vya wafanyakazi na mabaraza yao. Naagiza taasisi zote ambazo bado hazijaunda mabaraza ya wafanyakazi nchini zinapaswa kufanya hivyo. Lakini ninyi viongozi acheni migogoro ya kugombea madaraka, mara mnapelekana hadi mahakmaani, sitaki kuisikia,"amesema Waziri huyo.
Kutokana na kuibuka kwa malalamiko hayo, amesema suala hilo sasa litakomeshwa katika mapitio ya sheria yanayotarajiwa kupelekwa Bungeni wakati wowote, ili kuweka masharti ya kisheria na hatua kwa waajiri watakaokiuka.
Katika hatua nyingine, Waziri Sangu amewataka waajiri wa sekta binafsi kutekeleza kikamilifu amri ya kima cha chini cha mshahara iliyotangazwa na serikali, akieleza kuwa utekelezaji wake umefikia asilimia 90.
Amesema licha ya kiwango hicho cha utekelezaji, bado kuna waajiri ambao hawajatekeleza amri hiyo, akisisitiza kuwa serikali imepanga kuwaita waajiri wa baadhi ya sekta ambazo bado zina changamoto katika utekelezaji wa agizo hilo mwanzoni mwa mwezi Desemba.
Vilevile, amesema serikali itachukua hatua za kisheria dhidi ya waajiri watakaobainika kutotekeleza masharti ya kima cha chini cha mshahara.
Akitoa taarifa yake, Katibu Mkuu wa TUGHE, Rugemalila Rutatina, amesema baadhi ya taasisi, waajiri wake wanakwamisha uundaji wa mabaraza ya wafanyakazi, huku baadhi yao wakiwachagulia watumishi wapya wanaoajiriwa vyama vya kujiunga navyo.