Shirika la WHO lahofia kutofikiwa malengo ya maendeleo ya UN ya 2030

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema janga la Uviko-19 pamoja na vita na migogoro ni masuala yaliyorudisha nyuma juhudi za kuimarisha afya na ustawi wa wanawake pamoja na watoto.

Kwa mujibu wa data za WHO zilizowasilishwa katika mkutano wake wa kilele mjini Berlin, njaa pamoja na umasikini ni mambo yaliyoongezeka na kuna dalili za wazi za ongezeko la ndoa za utotoni, unyanyasaji na matumizi ya nguvu majumbani pamoja na maradhi ya msongo wa mawazo na kiwewe miongoni mwa watu wenye umri wa balekhe.

Takriban watoto milioni 21 duniani kote wamekosa chanjo katika mwaka 2021, idadi ambayo ni milioni 6 zaidi ya ile iliyoshuhudiwa mwaka 2019 kabla ya janga hilo kuzuka. WHO imesema ulimwengu hauko kwenye nafasi ya kuyafikia malengo ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030 ambayo ni pamoja na afya, lishe bora na elimu miongoni mwa mengine.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii