Wauguzi Wafutiwa leseni
Baraza la Wauguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), limewafutia leseni
wauguzi wasaidizi wawili wa Hospitali ya Wilaya ya Mkomaindo, Masasi
mkoani Mtwara, baada ya kupatikana na hatia ya uzembe uliosababisha
kifo cha majamzito na mtoto wake.
Wauguzi hao
Elizabeth Njenga na Pascal Mnyalu, walishtakiwa kwenye baraza hilo
pamoja na wauguzi wengine watatu na madaktari wawili, wote wa hospitali
hiyo kuhusika na uzembe uliopoteza maisha ya mjamzito Aisha Romanus.
Wauguzi
wengine waliofikishwa katika baraza hilo ni Joyce Nkane na Tumaini
Milanzi ambao walipewa onyo kali na Lucia Liababa, ambaye alifutiwa
shtaka lake baada ya kuonekana kutohusika moja kwa moja.
Kabla
ya hukumu hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Lilian Msele,
pia aliwatia hatiani madaktari wawili wa hospitali hiyo, Amina Mushi na
Hashimu Chiwaya, ambao taarifa zao zitapelekwa kwenye Baraza la
Madaktari ili hatua stahiki zichukuliwe.
Awali
dada wa marehemu Agnes John, alilieleza Baraza hilo kuwa Novemba mosi,
mwaka jana, mdogo wake Aisha, alishikwa na uchungu wa uzazi na kuamua
kumfikisha zahanati ya Lukuledi na muuguzi wa zahanati hiyo baada ya
kumpima aliwaeleza waende hospitali ya Wilaya ya Mkomaindo.
Alisema,
hata hivyo alipopiga simu hospitali hiyo ya wilaya wauguzi walimjibu
hawakuwa na mafuta ya kutumia kwenye gari la wagonjwa na kulazimika
kukodi bajaji ambayo pia iliharibika njiani na baada ya matengenezo
walifika saa moja usiku hospitali ya Mkomaindo.
Agnes
alisema baada ya kupokewa mgonjwa wake hakupata huduma haraka na
kuambiwa aondoke jambo alilolipinga na muda mfupi alimuona mdogo wake
akiomba msaada kwa wauguzi hao, lakini hawakumjali na ilipofika usiku wa
saa tano akaaga dunia.
Wajumbe wa baraza hilo
ambao waliwahoji madaktari na wauguzi hao walishangaa baada ya maelezo
yao kuwa tofauti kiasi cha mjumbe Haruna Neke kukerwa kutokana na
maelezo waliyoyawasilisha awali baada ya kutakiwa kuandika taarifa
kutofautiana na maelezo waliyokuwa wakiyatoa.
Kutokana
na hukumu hiyo Mwenyekiti wa baraza hilo, Lilian Msele, alisema wauguzi
hao hawatotakiwa kufanya shughuli zozote za kiuguzi kutokana na kukiuka
kanuni na viapo vyao walivyokula, pia alilaumu uongozi wa hospitali
hiyo kutokuawa na ufuatiliaji wa watumishi wake na iwapo usimamizi
ungekuwa mzuri maafa kama hayo yasingeweza kutokea.
Naye
Msajili wa Baraza hilo, Agnes Mtawa, aliwataka wananchi kufikisha
malalamiko yao waonapo hawatendewi haki na wauguzi na madaktari ili
wachukue hatua stahiki huku akibainisha kuanza kusikiliza kesi nyingine
iliyotoka mkoani Arusha.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii