Naibu
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe.Atupele Mwakibete ameitaka Bodi ya
Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), kuandaa Sera, Sheria, Kanuni na
miongozo bora itakayosimamia na kuleta maendeleo ya sekta ya ujenzi
nchini.
Akizindua
Bodi mpya ya NCC jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Mwakibete amesema
maendeleo endelevu katika sekta ya ujenzi nchini yatapatikana endapo
uwepo wa Sheria, Miongozo ya Majenzi, na Viwango Msawazo vya majengo na
nyumba za Serikali vitakuwepo na kuzingatiwa na wadau wote wa sekta ya
majenzi.
“Naagiza
zoezi hili lifanyike haraka, lakini kwa umakini na weledi kwa
kuwashirikisha wadau wote ili kuleta tija inayotarajiwa,” amesema
Mwakibete.
Aidha,
ameitaka Bodi hiyo kuandaa miongozo ya gharama za ujenzi wa miradi ya
barabara ili miongozo na sheria zote zitumike katika mwaka wa fedha ujao
wa 2023/2024.
“Ninavyozungumza
hivi sasa hatuna Sheria ya Majenzi, hatuna Miongozo ya Majenzi, hatuna
Kanuni za Majenzi. Hivyo mtaona kwamba mnayo mambo mengi ambayo
mnatakiwa kuyafanyia kazi kwa haraka ili kubadili mtazamo wa wadau na
Serikali juu ya Baraza la Taifa la Ujenzi,” alisisitiza Mwakibete.
Hata hivyo ameitaka NCC kufanya kazi kwa bidii ili kuleta ubunifu na tija katika sekta ya majenzi kwa ujumla.
"
Sekta ya ujenzi katika nchi yoyote ni sekta muhimu kwa jinsi
inavyochangia maendeleo ya uchumi wa nchi na kwa Tanzania sekta hii
inachangia wastani wa asilimia 14 za pato la Taifa kwa
mwaka,"amebainisha Naibu Waziri huyo.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo ya NCC Dakta, Fatma Mohamed
amesema Bodi hiyo itafanya kazi kwa bidii na kuleta mabadiliko chanya
kwa kuwa wajumbe wa Bodi hiyo ni wataalam waliobobea katika Sekta ya
Ujenzi.