Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema polisi nchini Qatar, imewakamata na kuwanyanyasa wanachama wa Jamii ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, kuelekea mashindano ya soka ya kombe la dunia mwezi ujao.
Mapenzi ya jinsia moja yameharamishwa katika taifa hilo la Ghuba ambalo limekuwa likichunguzwa juu ya rekodi yake ya haki za binaadamu, kabla ya mashindano hayo yanayotarajiwa kuvutia mashabiki milioni moja kutoka mataifa ya nje.
Huma Rights Watch imesema imerekodi visa sita vya watu kupigwa vibaya na visa vitano vya unyanyasaji wa kingono ndani ya vizuizi vya polisi kati ya mwaka 2019 na 2022. Kushiriki mapenzi nje ya ndoa, ushoga na usagaji havikubaliki nchini Qatar na anayekutwa na hatia anaweza kufungwa hadi miaka saba jela.
HRW imeliomba shirikisho la soka duniani FIFA kuishinikiza Qatar kufanya mabadiliko ya kuwalinda watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.