Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo imemfukuza balozi wa Rwanda nchini humo Vincent Karega. Hatua hiyo inajiri wakati kundi la waasi la M23 ambalo Kongo inadai kuwa linaungwa mkono na Kigali, likiendelea kupata nguvu huko mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa ya msemaji wa serikali ya Kongo Patrick Muyaya, imesema kuwa kutokana na Rwanda kuendelea kuunga mkono M23, baraza la ulinzi linaloongozwa na Rais Felix Tshisekedi limeamua kumpa balozi wa Rwanda Vincent Karega saa 48 kuondoka nchini humo.
Uamuzi wa kumtimua balozi wa Rwanda umefikiwa baada ya serikali ya Congo kufanya tathmini juu ya hali ya usalama nchini humo. Rwanda imekuwa ikikanusha kuliunga mkono kundi la M23, na imetaja kusikitishwa na hatua ya kufurushwa kwa Balozi wake.