Marekani yatangaza zawadi ya dola milioni 10 kwa atake kuwa na taarifa juu ya viongozi wa Al-Shabab

Marekani imesema itatoa zawadi ya hadi dola milioni 10 kwa yeyote ambaye atakuwa na taarifa kuhusu viongozi wakuu wa Al-Shabab, hatua iliyotokana na mfululizo wa mashambulizi mabaya ya kundi hilo la kigaidi. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeeleza kuwa, kwa mara ya kwanza itatoa donge nono kwa habari itakayowezesha kusaidia kutatiza mifumo ya kifedha ya kundi la Al-Shabab lenye mafungamano na Al-Qaeda.

Hivi karibuni wapiganaji wa Al-Shabab wameongeza mashambulizi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na maeneo mengine ya nchi hiyo kufuatia mashambulizi dhidi ya kundi hilo yanayofanywa na serikali mpya ya Rais Hassan Sheikh Mohamud.

Marekani imetangaza zawadi nono ya hadi dola milioni 10 kila mmoja kwa taarifa zozote juu ya maficho ya kiongozi wa Al-Shabab Ahmed Diriye, naibu wake Mahad Karate na Jehada Mostafa, raia wa Marekani anayesemakana kuwa na majukumu mbalimbali katika kundi hilo.

Kwa mujibu wa bango lililotolewa na Marekani likiwa na picha za watatu hao, Washington imesema viongozi hao wa Al-Shabab wamehusika na mashambulizi mengi ya kigaidi nchini Somalia, Kenya na mataifa jirani na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii