Mahakama ya rufaa Afrika Kusini yaamua Zuma arejeshwe jela

Mahakama ya rufaa nchini Afrika Kusini imesema msamaha uliotolewa kwa rais wa zamani Jacob Zuma, wa kuachiwa kwa ajili ya matibabu ulikuwa kinyume cha sheria, na kwamba Zuma anatakiwa kurudishwa jela kumaliza kifungo chake.

Zuma mwenye umri wa miaka 80, alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela mwezi Juni mwaka jana kwa kosa la kuidharau mahakama, kadhia iliyozua machafuko nchini Afrika Kusini.

Hata hivyo, alitumikia miezi miwili tu jela kabla ya kupewa msamaha kutokana na sababu za kiafya licha ya kamati ya matibabu kusema Zuma hakukidhi masharti ya kupewa msamaha huo. Kulingana na ripoti za kimatibabu zilizotajwa katika uamuzi wa mahakama ya rufaa, Zuma ana matatizo ya shinikizo la damu, viwango vya juu vya sukari na vidonda vya tumbo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii