Mfalme Charles wa III amemkaribisha kwenye kasri ya Buckingham rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa anayefanya ziara rasmi ya siku mbili nchini Uingereza. Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili. Ramaphosa na mkewe walilakiwa na mfalme Charles na mkewe Camilla kwa heshima ya gwaride la kijeshi.
Ramaphosa ambaye ni kiongozi wa kwanza wa taifa kufanya ziara rasmi nchini humo tangu Mfalme Charles alipochukua hatamu za madaraka pia atakutana na waziri mkuu Rishi Sunak na kulihutubia bunge. Ramaphosa anafanya ziara hiyo wakati Uingereza inatafuta njia ya kuimarisha zaidi mahusiano na Afrika Kusini ambayo ni mshirika wake mkubwa wa kibiashara barani Afrika.