Waziri wa ulinzi wa Poland, Mariusz Blaszczak ameiomba Ujerumani kuusafirisha kwenda Ukraine, mfumo wa ulinzi wa makombora aina ya Patriot uliokusudiwa kwenda Poland, ili kusaidia ulinzi dhidi ya uvamizi wa Urusi.Kupitia ukurasa wake wa Twitter, waziri huyo amesema hatua hiyo itasaidia Ukraine kujilinda dhidi ya uharibifu unaofanywa na Urusi, vikiwemo kukatika kwa umeme na kuimarisha usalama wa mpaka wao wa upande wa mashariki. Ahadi hiyo ya Ujerumani inafuatia tukio la mripuko mbaya wa kombora katika kijiji cha Poland wiki iliyopita ambao Warsaw inaamini kuwa huenda lilikuwa kombora la mfumo wa ulinzi wa anga wa Ukraine lililorushwa dhidi ya mashambulizi mengi ya Urusi.