Korea Kaskazini imeitaka Marekani na Korea Kusini kuacha kufanya luteka kubwa za pamoja za kijeshi inazozitaja kama uchokozi unaoweza kuchochea hatua kali zaidi kutoka kwa Pyongyang.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini jana imesema hali katika rasi ya Korea na viunga vyake kwa mara nyingine imeingia katika awamu ya kupambania mamlaka kutokana na hatua za Marekani na Korea Kusini kukataa kusitisha mazoezi hayo. Marekani na Korea Kusini wameanza luteka kubwa kabisa ya kijeshi jana Jumatatu inayojumuisha takriban ndege 240 za kivita.
Operesheni hiyo inatarajiwa kuendelea hadi siku ya Ijumaa, hii ikiwa ni kulingana na jeshi la Marekani. Marekani na Korea Kusini wanaoamini kwamba Korea Kaskazini huenda wakaanzisha tena majaribio ya makombora ya nyuklia yaliyofanyika kwa mara mwisho mwaka 2017, wanajiandaa kulidhibiti taifa hilo kupitia mazoezi hayo.