Jaji mmoja nchini Marekani ameitupilia mbali kesi dhidi ya Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kuhusiana na mauaji ya mwaka wa 2018 ya mwandishi habari Jamal Khashoggi.
Jaji John Bates amezungumzia kile
alichokiita wasiwasi kuhusiana na uamuzi wake lakini akasema ilimbidi
kufuata pendekezo la karibuni la Wizara ya Sheria ya Marekani kuwa bin
Salman apewe kinga ya kushitakiwa. Wasiwasi wa Bates ulitokana sio tu na
tuhuma za kuaminika za kuhusika kwa mwanamfalme huyo katika mauaji ya
Khashoggi, lakini pia na wakati wa uteuzi wa bin Salman kuwa waziri mkuu
wa Saudi Arabia. Kesi hiyo iliwasilishwa na mchumba wa Khashoggi,
Hatice Cengiz, ambaye anamtuhumu Rais wa Marekani Joe Biden kwa kumpa
kinga bin Salman.