Raila na Ruto kukutana leo katika kongamano la viongozi wa Afrika na Amerika
RAIS William Ruto leo Jumanne atakutana na kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga, nchini Amerika wanapohudhuria Kongamano la Amerika la Viongozi wa Afrika linaloanza leo jijini Washington DC.
Bw Odinga aliondoka nchini Jumamosi kuhudhuria kongamano hilo, huku Rais Ruto akiondoka Jumatatu baada ya kuongoza sherehe za Sikukuu ya Jamhuri.
Bw Odinga alisusia maadhimisho hayo, baada ya kutishia kuandaa sherehe ya upinzani ya Jamhuri katika uwanja wa Jacaranda, Nairobi.
Hata hivyo, alifutilia mbali mpango huo katika siku za mwisho mwisho, akitaja kongamano hilo kama sababu ya kutoongoza sherehe hizo.
Wiki iliyopita, Bw Odinga alitishia kuongoza maandamano makubwa dhidi ya serikali ya Rais Ruto, akiikosoa kwa kushindwa kupunguza gharama ya maisha, kuwatishia makamishna waliojiuzulu kutoka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), mapendeleo kwenye uteuzi wa nyadhifa kuu serikalini, kupinga mpango wa kuagiza magunia milioni 10 ya mahindi yaliyofanyiwa ukarabati wa kisayansi maarufu kama GMO.
Kongamano hilo litaanza leo Jumanne na kukamilika Alhamisi, huku lengo kuu likiwa kuboresha ushirikiano baina ya Amerika na Afrika.
Bw Odinga anahudhuria kongamano hilo kama Balozi Mkuu wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu miundomsingi.
Wakati wa kuahirisha mkutano uliofaa kufanyika jana Jumatatu, Bw Odinga alisema kuwa sababu ilikuwa kualikwa na Rais Joe Biden wa Amerika kwenye kongamano hilo la siku tatu.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii