Wabunge wa Ulaya wamvua Eva Kaili umakamu rais

Makamu Rais wa Bunge la Ulaya, Mgiriki Eva Kaili, ameondolewa kwenye nafasi hiyo baada ya tuhuma za kupokea rushwa. 

Bunge lilipiga kura hapo jana asubuhi ya kumuondowa Kaili kutoka nafasi yake ya kuwa mmoja wa makamu wa 14 rais.

Hoja ya kumuondowa madarakani iliungwa mkono na wabunge 625 wa Bunge la Ulaya, dhidi ya mmoja aliyepinga na wawili waliojizuwia kupiga kura zao.

Thuluthi mbili ya wabunge walikuwa wanahitajika kumzuia kuwa mmoja wa makamu 14 wa rais wa bunge hilo.

Mbunge huyo mwenye umri wa miaka 44 kutokea chama cha Kisoshalisti cha Ugiriki alikamatwa siku ya Ijumaa nchini Ubelgiji.

Anatuhumiwa kuwa sehemu ya kundi lililokubali rushwa kutoka Qatar ili kushawishi sera zinazolinufaisha taifa hilo dogo la Ghuba.

Tayari Kaili ameshavuliwa kinga yake na kwa sasa yuko kizuizini. Undani zaidi wa mashitaka yanayomkabili yatatangazwa leo, kwa mujibu wa maafisa wa Ubelgiji.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii