Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo, amezindua josho la kuogeshea mifugo katika Kijiji cha Irkujit wilayani Simanjiro mkoani Manyara ambalo limejengwa kupitia mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR).
Akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya kukagua mradi huo amewapongeza wananchi hao kwa kuibua mradi huo ambao unawawezesha kuikinga mifugo yao kwa magonjwa yaenezwayo na kupe na mbung’o.
Dkt. Jafo amesema josho hilo linalotarajiwa kuhudumia wananchi takriban 30,000 wa kijiji hicho na vijiji jirani ni matunda ya serikali katika kuhakikisha inawasidia wananchi kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
"Ndugu zangu leo hii ukienda Mto Ruaha ambao ndio chanzo cha maji kinachopeleka katika Bwawa la Mtera umekauka, pia Kidatu maji yamepungua na ndio maana tumeshuhudia baadhi ya maeneo yanapata mgao wa umeme, hayo yote ni mabadiliko ya tabianchi," amesema Dkt. Jafo.
Aliweka bayana kuwa ili kukabiliana na changamoto kama hizo, Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza mradi wa EBARR katika baadhi ya vijiji ambavyo vinakabiliwa na changamoto ya ukame ili kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo.
Waziri huyo ameupongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa kuisimamia mradi hiyo katika eneo lao huku akitoa rai kwa wananchi wa Wilaya ya Simanjiro kuitunza ili isiharibiwe na idumu kwa ajili ya vizazi vijavyo.