Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis amefichua kwa mara ya kwanza kuwa alisaini barua ya kustaafu karibu muongo mmoja uliopita, iwapo afya yake itakuwa mbaya na kumzuia kuendelea na majukumu yake. Francis -- ambaye amefikisha umri wa miaka 86 jana Jumamosi -- alisema katika siku za nyuma kuwa angejiuzulu wadhifa wa upapa kama matatizo ya kiafya yatamzuia kutekeleza majukumu yake.
Katika mahojiano na gazeti la Uhispania la ABC, kiongozi huyo wa kanisa katoliki amesema alisaini barua ya kujiuzulu na kumpa waziri wa mambo ya kigeni wa Vatican, Tarcisio Bertone, kabla ya kadinali huyo kujiuzulu mwaka wa 2013. Ameongeza kuwa hajui Bertone, aliifanyia nini barua hiyo.
Francis anasumbuliwa na tatizo la goti ambalo limemlazimu kutumia kiti cha walemavu katika miezi ya karibuni.