Mkurugenzi mkuu wa Twitter Elon Musk amesema atajiuzulu nafasi hiyo baada ya kumpata mrithi kufuatia kura ya maoni aliyoianzisha iliyoonyesha watumiaji wanamtaka aachie wadhifa huo.
Matokeo ya kura hiyo yaliyochapishwa siku ya Jumatatu yalionyesha asilimia 57 ya wapiga kura sawa na watumiaji milioni 10 walimtaka Musk kuachia ngazi wiki chache tu baada ya kuchukua umiliki wa kampuni hiyo aliyoinunua kwa dola bilioni 44.
Bilionea huyo amekuwa akitumia kura za maoni kwenye mtandao huo kufanya baadhi ya maamuzi ikiwa ni pamoja na kurejeshwa kwa ukurasa wa aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump na watumiaji wengine walisimamishwa, kuwaondoa waandishi wa habari na kujaribu kutoza fedha huduma ambazo awali zilitolewa bure.