Marekani, Japan na Korea Kusini zimeweka vikwazo vipya kwa watu binafsi na mashirika ya Korea Kaskazini kujibu majaribio ya makombora ya hivi karibuni nchini humo. Hatua za Marekani zilizotangazwa jana, zinazuia mali yoyote ya maafisa watatu wa Korea Kaskazini nchini Marekani, hatua kubwa ya ishara dhidi ya nchi iliyojitenga ambayo imekaidi shinikizo la kimataifa juu ya mipango yake ya silaha.
Wizara ya fedha ya Marekani pia ilitishia vikwazo dhidi ya mtu yeyote ambaye atafanya biashara na Jon Il Ho, Yu Jin na Kim Su Gil, ambao walitambuliwa kuhusika moja kwa moja katika utengenezaji wa silaha. Katika taarifa, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, amesema kuwa majaribio ya makombora ya hivi karibuni kutoka Korea Kaskazini, yanahatarisha usalama wa eneo hilo na dunia nzima.