Kwa mujibu wa msemaji wake rais huyo anayekabiliwa na kashfa na kitisho cha kuondolewa madarakani hana nia ya kujiuzulu na kwamba ataendelea kupambana kisiasa na kwa njia za kisheria.
Ramaphosa amekuwa akikabiliwa na shutuma tangu mwezi Juni, baada ya mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi alipowasilisha malalamiko kwa polisi akidai kuwa rais huyo hakuripoti polisi wizi uliotokea mwezi Februari mwaka 2020 katika shamba lake kaskazini mashariki mwa nchi.
Katika malalamiko hayo Ramaphosa pia anadaiwa kuwa alipanga juu ya kutekwa nyara wezi hao na kisha kuwahonga ili wanyamaze kimya.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amekana kufanya makosa yoyote lakini kashfa dhidi yake na taarifa za kupatikana zaidi ya dola nusu milioni zilizofichwa kwenye mito ya makochi, zimetolewa wakati mbaya kwake kutokana na kwamba mnamo Desemba 16, Ramaphosa atagombea kwenye uchaguzi wa rais wa chama tawala cha ANC nafasi ambayo ni muhimu katika kumwezesha kuendelea kusalia kama rais wa taifa la Afrika Kusini