Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amesema jana kwamba wafuasi wa mtangulizi wake Jair Bolsonaro waliovamia majengo ya serikali huenda walipatiwa msaada na mtu wa ndani.
Lula mwanasiasa wa mrengo wa kushoto amenukuliwa akisema mbele ya waandishi wa habari mjini Brasilia kwamba ana uhakika wavamizi hao walifunguliwa mlango wa ikulu na kuingia kwa sababu hakukuwa na milango iliyovunjwa.
Amesema tayari ameagiza uchunguzi wa kina kwa watumishi wa makazi hayo ya rais. Wavamizi hao walifanikiwa kuingia kwenye majengo ya makazi ya rais, bunge na mahakama ya juu, siku ya Jumapili wakidai kughadhabishwa na ushindi wa Lula da Silva dhidi ya kiongozi wao Bolsonaro wa mrengo wa kulia. Lula aidha amesema uvamizi huo ni onyo zito na kuahidi kuchukua hatua kali na kuwa waangalifu zaidi katika siku za usoni.