Chebukati Asema Hajuti Anapoondoka Afisini Januari 17, 2023

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati amesema hajuti anapoondoka afisini baada ya kuhudumu kwa miaka sita.

Atastaafu rasmi mnamo Januari 17, 2023, kwani Katiba hairuhusu muda wa kuhudumu kwa makamishna kuongezwa kwa zaidi ya miaka sita.

Bw Chebukati mnamo Ijumaa, Desemba 23, 2023, alisema anaonea fahari muda aliohudumu kileleni mwa tume hiyo ambapo aliongoza chaguzi kuu mbili.

“Sina majuto. Nilitoa mchango wangu katika kutekeleza mageuzi bora katika tume. Yule ambaye atachukua usukani anafaa kuendeleza mageuzi hayo,” Bw Chebukati akasema Ijumaa katika mkutano uliandaliwa na Kamati Shirikishi ya Vyama vya Kisiasa, katika Chuo cha Utalii.

Mwenyekiti huyo, hata hivyo, alisema IEBC ilipitia changamoto nyingi kabla na hata wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, ambazo zinafaa kushughulikiwa na mwenyekiti mpya atakayeteuliwa na makamishna wenzake.

“Mojawapo ya changamoto tuliyokumbana nayo ni ya kifedha. Serikali inafaa kutoa pesa kwa IEBC mapema ili iweze kufanya maandalizi ya mapema. Haifai kutuma pesa katika mwaka wa mwisho jinsi ilivyofanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022,” Bw Chebukati akasema.

Aidha, mwenyekiti huyo alisema mageuzi yanayohusu sheria za kuimarisha usimamizi wa uchaguzi zinafaa kuimarishwa sawa na kuimarishwa kwa teknolojia ya upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi, haswa ule wa urais.

Hata hivyo, mapungufu ya uongozi wa Bw Chebukati yalidhihirika kufuatia kufutiliwa mbali kwa matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2017 na Mahakama ya Juu.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa uchaguzi wa urais kufutuliwa mbali nchini Kenya, na mara ya pili kwa hali kama hiyo kushuhudiwa barani Afrika.

Bw Chebukati aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo mnamo Januari 17, 2017 baada ya kupendekezwa kwa wadhifa huo mwezi mmoja uliotangulia.

Mwenyekiti huo na makamishna sita walichukua usukani kutoka kwa mtangulizi wake, Ahmed Issack Hassan na wenzake waliolazimishwa kujiuzulu.

Bw Chebukati anaondoka  IEBC pamoja na makamishna Profesa Abdi Guliye na Boya Molu, wawili kati ya makamishna sita walioteuliwa pamoja naye 2017.

Wengine wanne walijiuzulu baada ya uchaguzi mkuu wa 2017. Wao ni aliyekuwa naibu mwenyekiti Consolata Nkatha, Paul Kurgat, Margaret Mwachanya na Roselyn Akombe.

Bw Chebukati pia alivitaka vyama vya kisiasa kuendesha kura za michujo kwa njia huru, haki na itakayoaminika kama hatua mojawapo ya kujenga demokrasia ya ndani.

“Hili likifanyika idadi ya wanasiasa wanaowania viti kama wagombeaji huru itapungua,” Bw Chebukati akasema

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii