Sudan Kusini kupeleka wanajeshi 750 nchini DRC

Sudan Kusini itapeleka wanajeshi 750 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku chache zijazo, watakaoungana na wenzao wa kikosi cha kikanda cha Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kukabiliana na mashambulizi ya waasi, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa jeshi hilo jana Jumatano.

Meja Jenerali Lul Ruai wa Jeshi la ulinzi la Sudan Kusini, SSPDF, amesema akiwa mjini Juba kwamba wanajeshi hao mahiri 750 wamekuwa wakipata mafunzo kwa zaidi ya miezi sita wakijiandaa kwenda nchini humo.Akizungumza mjini Juba, Rais Salva Kiir aliwataka wanajeshi hao kulinda usalama, raia pamoja na mali zao ili zisiharibiwe.

Shughuli hii inafanyika ikiwa ni miezi minne tangu maelfu ya wanamgambo ambao ni pamoja na waasi wa zamani watiifu kwa Kiir na mpinzani wake Rieck Machar kutangamana kwenye jeshi la Sudan, ikiwa ni moja wapo ya kipengele muhimu cha utekelezaji wa makubaliano ya amani ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii