Luiz Inacio Lula da Silva ameapishwa kuongoza kwa muhula wa tatu kama rais wa Brazil.
Lula aliapa jana kuwapigania watu maskini na utunzi wa mazingira na kuijenga upya nchi baada ya utawala wa kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia Jair Bolsonaro kuigawa nchi hiyo.
Mwanasiasa huyo mkongwe wa siasa za mrengo wa kushoto mwenye umri wa miaka 77, ambaye awali aliiongoza Brazil kuanzia 2003 hadi 2010, aliapa mbele ya Bunge, akirejea katika ulingo wa kisiasa ikiwa ni chini ya miaka mitano baada ya kufungwa jela kutokana na mashitaka yenye utata na ambayo yalifutwa ya rushwa.
Lula alisema serikali yake itafanya kazi ya kufuta urithi wa kuzorota kwa uchumi, kuongezeka kwa umaskini na kupunguzwa kwa ufadhili katika sekta za afya, elimu na sayansi.