Shule katika miji miwili mikubwa nchini Malawi zitasalia kufungwa hadi wakati usiojulikana kutokana na mripuko wa kipindupindu unaoendelea kuwa mbaya zaidi. Wanafunzi walitarajiwa kurudi madarasani jana baada ya mapumziko.
Lakini wizara ya afya imesema kuanza kwa mihula kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika mji mkuu Lilongwe na mji wa kusini Blantyre kutacheleweshwa kwa angalau wiki mbili.
Waziri wa Afya Khumbize Chiponda amesema katika taarifa kuwa kuahirishwa huko kumetokana na kuongezeka kwa idadi ya visa vya kipindupindu na vifo.
Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika imerekodi takriban visa 18,000 vya ugonjwa huyo na vifo 595 tangu Machi mwaka jana katika kile Umoja wa Mataifa unasema ni mripuko mkubwa kabisa kuwahi kulikumba taifa hilo katika miaka kumi.