RAIS wa Amerika, Joe Biden, amesifu utawala wake akisema ameweza kutekeleza baadhi ya ahadi zake.
Akizungumza bungeni wakati wa hotuba yake ya pili kuhusu hali ya taifa la Amerika Jumanne usiku, Rais huyo alipongeza mafanikio yake ya kisheria na kisera.
“Hali ya taifa imeimarika. Hii ni kwa sababu ya umoja na ushirikiano baina ya wananchi na viongozi wao,” akasema Rais Biden.
“Huu umekuwa mtazamo wangu wa nchi yetu kila wakati, na najua ni mtazamo wa wengi kati yenu. Kuboresha taifa hili na kuinua uchumi wa Amerika,” akaongeza Biden.
Biden alizungumza kwa kirefu na kwa undani akisema kwamba lengo lake kuu ni kuwahusisha wananchi kujenga uchumi.
“Tunajenga uchumi ambapo hakuna mtu atakayeachwa nyuma. Wengi pia wamepata nafasi za ajira. Hii itatufanya tusonge mbele kama taifa.”
Biden alisema utawala wake ulibuni nafasi mpya za ajira milioni 12.
Baadhi ya mafanikio aliyoyataja Rais huyo wa Amerika ni jinsi alivyopambana na janga la Corona.
“Miaka miwili iliyopita, janga la corona liliathiri sekta mbalimbali ikiwemo biashara, masomo na hata kuwaacha wengi bila ajira. Hata hivyo, ni jambo la kusherehekea kwa kuwa nchi yetu iliweza kusimama imara na kupambana na janga hilo hatari,” akasema Biden.
Ili kupambana na janga la corona, Biden aliwapa changamoto wananchi wa Amerika kuvaa barakoa kwa siku 100. Hatua hiyo iliungwa mkono na wananchi, jambo lililosaidia pakubwa kupunguza maambukizi ya virusi vya corona katika nchi hiyo.
Baada ya kula kiapo kama Rais wa Amerika, Biden alitia saini maagizo 17, tisa kati yao ni mabadiliko ya moja kwa moja ya sera zilizotungwa na Donald Trump.
Biden pia amejaribu kurejesha umoja na ushirikiano, ulioonekana kuvurugwa na utawala wa Trump.