Anayeidai TRA Shilingi milioni 986 adai kutishiwa maisha

 Kwa takribani miaka sita sasa, mfanyabiashara Ramadhani Ntunzwe ‘Babu Rama’, ameendelea kupaza sauti kudai fidia ya Sh986 milioni kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), huku akidai kutishiwa maisha na watu wanaodaiwa kuwa maofisa wa mamlaka hiyo.

Mfanyabiashara huyo kwa mara ya kwanza aliwasilisha kilio chake Februari 28, 2019 katika kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wafanyabiashara wa Ilala ikiwa ni miezi saba tangu alipokutana na mkasa huo Oktoba 30, 2016 alipokuwa akisafirisha mzigo wake kutoka Afrika Kusini kupitia mpaka wa Tunduma kuelekea Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, Ntunzwe alieleza mikasa miwili iliyomkuta dhidi ya TRA; kwanza kushikilia mzigo wake kwa miaka mitatu kwa tuhuma za kukwepa kukodi huku yeye akidai kukataa kutoa rushwa ya Sh2milioni na mkasa wa pili ni kuibiwa mali zake zenye thamani ya Sh986 milioni katika duka lililopo Kariakoo baada ya TRA kulifunga kwa madai ya kutotumia mashine ya EFD.

Katika kikao hicho, Majaliwa aliagiza mfanyabiashara huyo arudishiwe mzigo wake baada ya kujiridhisha huku akiagiza ofisa wa TRA akamatwe. Miezi minne baadaye, Rais John Magufuli aliagiza TRA kuhakikisha wanalipa fidia zake, wakati huo Makamu wa Rais akiwa Samia Suluhu Hassan.

Wiki iliyopita Ntunzwe alijitokeza mbele ya wanahabari kumuomba Rais Samia kuingilia kati madai hayo, ili alipewe fidia yake hiyo inayotokana na hasara ya upotevu wa mali zilizoibiwa dukani kwake Kariakoo.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema majadiliano kati ya mfanyabiashara huyo na TRA yanaendelea ikiwamo masuala ya madai yake. “Hadi wiki hii mfanyabiashara huyo alikuwa anaendelea na mawasiliano na watalaamu wetu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii