KUFUTIA AGIZO LA RAIS SAMIA,CRDB BANK WAFANYA HILI SUALA LA RIBA KWA WAKULIMA NA WAFANYAKAZI






Benki ya CRDB January 24, 2022 imetangaza punguzo kubwa la riba katika mikopo kwa kundi la wakulima pamoja na wafanyakazi.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema punguzo hilo la riba linakuja kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mabenki kuhusu kupunguza riba ili kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Nsekela amesema katika punguzo hilo, riba ya mikopo ya kilimo imepunguzwa hadi 9% kutoka 20% iliyokuwa ikitozwa hapo awali, huku riba ya mikopo ya wafanyakazi ikipunguzwa kutoka 16% hadi kufikia asilimia 13%.

Punguzo hilo la riba, linatoa ahueni kwa wateja wa Benki ya CRDB kulipa mikopo yao kwa ribanafuu, viwango vya chini zaidi vya marejesho ya awali, pamoja na kupata wigo mpana wa kukopa.

“Kwa ushirikiano mkubwa na Benki Kuu ya Tanzania ambae ndie msimamizi wa sekta ya benki nchini, mwishoni mwa mwaka jana tuliweza kukaa chini na kuanza utekelezaji wa mchakato wa kupitia upya riba za mikopo mbalimbali inayotolewa na Benki yetu na hivyo ninajivunia kuona leo hii tumekuja na suluhisho la kilio cha muda mrefu cha wateja wetu,” amesema Nsekela huku akiwahamasisha wateja na Watanzania kuchangamkia fursa hiyo.

Kwa upande wa mikopo ya kilimo Nsekela amesema punguzo hilo la hadi 9% ni kubwa kupata kutokea katika soko, huku akibainisha kuwa benki hiyo imetoa punguzo hilo ili kusaidia kuimarisha sekta ya kilimo ambayo huchangia 26% ya pato la Taifa na kutoa ajira kwa 75% ya Watanzania.

“Lengo letu ni kuchochea kasi ya mapinduzi katika sekta ya kilimo nchini kwa kuwawezesha wakulima wadogo na wakati kufanya kilimo cha kisasa kupitia mikopo nafuu ya pembejeo na zana za kilimo,” amesema Nsekela.

Akielezea punguzo la riba kwa mikopo ya wafanyakazi, Nsekela amesema benki hiyo imejipanga kuendelea kuboresha ustawi wa wafanyakazi nchini kupitia mikopo ya riba nafuu.

“Wafanyakazi ni kundi muhimu kwa Benki yetu ndio maana tumekuwa tukiboresha kwenye riba ya mikopo ya kundi hili kila mwaka ili kuwasidia kufikia malengo waliyojiwekea jambo ambalo litaongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi,” amesema Nsekela.

Nsekela amewataka wafanyakazi kuchangamkia fursa hiyo ya kushuka kwa riba kuimarisha kuboresha maisha yao kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi, huku akiwaasa kutokopa bila ya kuwa na malengo.

“Hii ni mara ya tatu ndani ya miaka mitano iliyopita kwa Benki yetu kupunguza riba ya mikopo ya wafanyakazi, matarajio yetu ni kuwa wafanyakazi watachangamkia fursa hii ili kuboresha maisha yao na hilo ndo haswa lengo la Benki ya CRDB.” amesema Nsekela.

“Viwango vikubwa katika tozo za mikopo imekuwa changamoto kwa watanzania wengi hasa wale wa daraja la kati na la chini lakini sasa tunaamini kuwa hata wale ambao hawakuweza kukopa sasa watatumia fursa hii kuboresha biashara zao na maisha yao kwa ujumla.

Lakini pia tunaamini ndiyo maono hasa ya Mheshimiwa Rais kuona Watanzania wakishiriki kwa wingi katika shughuli za kiuchumi,” aliongeza Nsekela.

CRDB YAPATA TUZO KUTOKA MAREKANI MKURUGENZI ANENA “BENKI NYINGI ZILIPATA CHANGAMOTO, COVID 19 DUNIA”

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii