Putin aridhishwa na juhudi za China kumaliza mzozo nchini Ukraine

Rais wa Urusi Vladmir Putin ameeleza kuridhishwa na juhudi za mwenzake wa China Xi Jinping kuhakikisha suluhu ya mzozo wa Ukraine inapatikana.

Katika kikao kati ya viongozi hao jijini Beijing, rais wa China amesema ana matumaini makubwa kwamba uthabiti na imani itarejea barani Ulaya.

Aidha Xi ameeleza kuwa nchi yake itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha hilo linatendeka hivi karibuni.

Mwaka uliopita, China ilipendekeza masuala kadhaa yaliolenga kusaidia katika kumaliza mapigano yanayoendelea nchini Ukraine.

“China ina matumaini ya kurejea kwa amani na uthabiti barani Ulaya na itakuwa nguzo muhimu katika kufanikisha hilo.” Alisema rais Xi.

Aidha Putin amesisitiza kwamba nchi yake inaishukuru Beijing kwa mapendekezo yake ya kudhibiti hali ya mambo huko Kyiv.


China imekuwa nguzo muhimu kwa Urusi tangu ilipoivamia jirani yake nchi ya Ukraine ambapo imeendelea kuipa vifa muhimu inavyohitaji katika uzalishaji wa silaha.

Vile vile hatua ya China kununua mafuta kutoka nchini Urusi, kwa sehemu kubwa imesaidia katika ukuzaji wa uchumi wa Moscow.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii