Burundi: Mwili wa rais wa zamani Pierre Buyoya warejeshwa nyumbani

Mwili wa rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya, aliyefariki kutokana na UVIKO-19 mnamo mwezi Desemba 2020 huko Paris, ambako alikuwa amewasili tu kwa matibabu, na kuzikwa awali huko Bamako nchini Mali ambako alikuwa Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Afrika kwa muda mrefu, uko njiani kuelekea Burundi ambako atazikwa upya, kwa makubaliano utawala wa Burundi.

Mara mbili rais wa Burundi, kuanzia mwaka 1987 hadi 1993 na 1996 hadi 2003 na kila mara kwa hiari kukabidhi madaraka kwa mpinzani, mkuu huyo wa zamani wa nchi aliigawa Burundi kila wakati. Takriban miaka minne iliyopita, familia yake ililazimika kumzika "kwa muda" rais wa zamani wa Burundi huko Bamako, nchi yake ya pili kama alivyopenda kusema.


Wakati huo mahusiano yake yalikuwa mabaya zaidi na serikali ya Gitega, ambayo ndiyo kwanza ilikuwa imemhukumu kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya Melchior Ndadaye (mnamo mwezi Oktoba 1993), rais wa kwanza kutoka kabila la Wahutu aliyechaguliwa kidemokrasia, miezi mitatu baada ya kumkabidhi mamlaka. Pierre Buyoya siku zote alikuwa akikanusha kushiriki katika uhalifu huu ambao uliitumbukiza Burundi katika vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miaka 10.


Mazishi yamepangwa kufayika Rutovu kwa faragha ya familia

"Familia iliomba na kupata idhini kutoka kwa mamlaka ya Burundi kurudisha mwili wake na kuuzika upya katika nchi yake ya asili," kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa kwa umma Jumatatu jioni, wakati mwili wa Pierre Buyoya unatarajiwa kuwasili mjini Bujumbura mapema mchana.


Mawasiliano ya kwanza na rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, yalifanyika miezi michache baada ya kuapishwa kwake. Aliweza kumpokea mtoto wa kiume wa Pierre Buyoya, Olivier, katika ikulu yake mjini Bujumbura, mwaka mmoja tu baada ya kutawazwa kwake. Na ni Évariste Ndayishimiye mwenyewe ambaye alitoa idhni kwa ajili ya kurejesha mwili wa rais wa zamani, kulingana na vyanzo vyetu. Sharti pekee lililowekwa, hakuna sherehe rasmi kwa mazishi ya rais huyo wa zamani.

Baada ya kuwasili mjini Bujumbura, mwili wa Pierre Buyoya utasafirishwa hadi kwenye kilima chake cha asili cha Rutovu, kusini mwa nchi ambako atazikwa upya "katika faragha ya kifamilia", kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii