Watu milioni 10 waliokimbia makazi yao, wakimbizi milioni 3 na zaidi ya watu milioni 25 - nusu ya idadi ya watu - wanakabiliwa na uhaba wa chakula. Wakati nchi hiyo ikitumbukia katika "moja ya majanga mabaya zaidi" kulingana na Umoja wa Mataifa, idadi kubwa ya shughuli za kibinadamu zimekatizwa kutokana na ukosefu wa usalama.
Hali ni mbaya hasa katika mji mkuu Khartoum, katika mikoa ya Kordofan, Al-Jazirah na hasa Darfur, anaeleza Daktari Shible Sabhani, mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Sudan.
“Sababu kuu ya watu kuondoka Sudan ni njaa. Sio kwa sababu ya kutokuwa na usalama, au ukosefu wa huduma ya matibabu, lakini kwa sababu tu hakuna kitu cha kula. Mwanamke niliyekutana naye mpakani aliniambia: "Kidogo tulichokua tunakula kilichukuliwa na askari. Kwa hiyo hatuna la kufanya ila kuondoka nchini." Alitembea kwa siku tatu hadi mpaka wa Chad na watoto wake, bila kula chochote. "
Bila upatikanaji wa haraka wa misaada ya kibinadamu nchini humo, kutakuwa na maafa. Na hasa nataka kuzungumza kuhusu El Fasher ambapo karibu watu 800,000 wamezingirwa bila msaada wowote wa kibinadamu.
Malori saba ya misaada kwa sasa yanaelekea Darfur na El Fasher, anasema mwakilishi wa WHO nchini Sudan. Anatumai kuwa majadiliano yanayoendelea Geneva yatawezesha kupata usitishaji mapigano wa ndani na kufungua maeneo salama ya kibinadamu.
Tangu kuanza kwa mzozo huo, wapiganaji hao wameshutumiwa kwa kupora na kuzuia kimfumo misaada ya kibinadamu. Kutokana na hali ya dharura - hasa chakula - shiŕika la Madaktari Wasio na Mipaka linatoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na Umoja wa Mataifa kuŕejea Sudani, mashiŕika mengi yameondoka nchini humo kutokana na vita ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa miezi 15.