Nchini Uganda, mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine amesema maofisa wa usalama wamezingira makao makuu ya chama chake.
Hatua hii inakuja kuelekea maandamano yaliopangwa kufanyika siku ya Jumanne ya wiki hii kupinga kile wanaharakati wanasema ni kukithiri kwa ufisadi.
Tayari polisi katika taifa hilo la Afrika Mashariki wamepiga marufuku maandamano hayo.
Ripoti ya maofisa wa usalama kuzingira makao makuu ya chama chake Bobi Wine imekuja pia ikiwa imepita siku mbili tangu rais Yoweri Museveni, kuwaonya wanaopanga kuandamana kwamba wanacheza na moto.
Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, amewambia wanahabari kwamba makao makuu ya chama chake cha National Unity Platform (NUP) katika eneo la Kavule, nje na mji mkuu wa kampala yalikuwa yamezingirwa.
Mamlaka nchini Uganda imekuwa ikikabiliana vikali na chama cha NUP chake Wine mwanamuziki wa zamani ambaye alishindwa na rais Museveni katika uchaguzi wa 2021.