NAIBU wa rais nchini Amerika na mgombeaji wa kiti cha urais Kamala Harris, achangiwa $200m za kufanya kampeni.
Hali hiyo ilitokea baada ya rais wa Amerika Joe Biden kutangaza kusitisha azma yake ya kuwania urais dhidi ya mpinzani wake anayepeperusha bendera kwa tiketi ya Republican na ambaye kadhalika alikuwa rais wa Amerika, Donald Trump.
Biden alimpisha Kamala kuwa mpeperushaji bendera akiwania urais akiwa katika chama cha Democratic.
Kamati ya kuongoza kampeni ya Kamala ilitangaza jumla ya pesa zilizokusanya za kampeni kufikia siku ya Jumapili.
Aidha, kamati hiyo iliongeza kwamba kati ya pesa hizo zilizokusanywa, asilimia 66 ya waliochanga ni wahisani waliojitolea kuchanga peza za kampeni kwa mara ya kwanza katika mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2024.
Isitoshe, zaidi ya wahisani 170,000 wamejitolea bila malipo kumsaidia Kamala katika shughuli za kumpigia debe.
“Kasi alio nayo pamoja na nguvu ni ishara tosha kwamba Kamala amejituma kuwania urais. Ni kinyang’anyiro kitakachokuwa kikiamuliwa na idadi ndogo ya kura kutoka katika maeneo machache tu,” akasema mkurugenzi wa mawasiliano kitengo cha kampeni, Michael Tyler.
Kwa upande mwingine, kitengo cha mawasiliano cha mwaniaji wa urais Donald Trump kiliambia wanahabari kwamba mapema mwezi Julai mwaka huu, kilikuwa kimechanga $331 milioni katika kipindi cha miezi mitatu, na kupiku $264 milioni, pesa ambazo ziikuwa zimechangishwa katika kampeni ya rais Biden na wanachama wa mrengo wake wa chama cha Democratic katika muda sawa wa miezi mitatu.
Kamati ya kampeni ya Trump ilikuwa imekusanya $284.9m pesa tasilimu ikifika mwisho wa Juni mwaka huu huku, nao mrengo wa Democratic ukikusanya pesa taslimu $240m wakati huo.
Aliyekuwa spika katika bunge la Amerika, Nancy Pelosi, Kiongozi wa walio wengi katika bunge la Seneti, Chuck Schumer, Kiongozi wa wengi, Hakeem Jeffries, kiongozi wa walio wachache Jim Clyburn, aliyekuwa rais wa Amerika Bill Clinton na aliyekuwa katibu katika ikulu ya rais Hillary Clinton ni miongoni mwa viongozi waliotangaza kumuunga mkono Kamala.