Mkuu wa Jeshi la Iran asifia kibali cha kukamatwa kwa Netanyahu

Mkuu wa jeshi la Iran, Jenerali Hossein Salami ametaja hatua ya mahakama ya ICC kutoa vibali vya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wake wa ulinzi Yoav Gallant kama “mwisho na kifo cha kisiasa” cha Israeli.

Katika hotuba yake, kiongozi huyo amekaribisha hatua ya ICC akisema ni ushindi mkubwa kwa wapiganaji wa Palestine na wale wa nchini Lebanon, makundi yanayoungwa mkono na Iran.

Israel na washirika wake wamekosoa hatua ya ICC ya kutangaza kibali cha kukamatwa kwa Benjamin Netanyahu pamoja na Waziri wa zamani wa ulinzi Yoav Gallant.

Mahakama hiyo pia imetoa hati ya kukamatwa kwa mkuu wa kijeshi wa wapiganaji wa Hamas Mohammed Deif.

Netanyahu na Gallant wanatuhumiwa kwa kutekeleza makosa ya uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu katika Ukanda wa Gaza kwenye oparesheni zao za kujibu shambulio la Hamas la tarehe 7 ya mwezi Oktoba mwaka wa 2023.

Netanyahu tayari amelani hatua hiyo ya ICC, washirika wa Israeli ikiwemo Marekani nao pia wakiikosoa.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la  Amnesty International kwa upande wake limekaribisha tangazo la ICC. Kwa sasa mataifa wanachama 124 wa ICC yanauwezo wa kumkamata Netanyahu iwapo atazuru nchi hizo.

Tayari mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Karim Khan amezitaka nchi wanachama na zile ambazo sio wanachama kushirikiana kuhakikisha wanaheshimu sheria ya kimataifa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii