Familia ya ukoo wa Qaresi imetangaza kifo cha mwanasiasa mkongwe na kiongozi wa muda mrefu wa serikali, Mateo T. Qaresi, aliyefariki dunia tarehe 8 Julai 2025 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Lucy Qaresi Uisso, mtoto wa tatu wa marehemu, wakati akizungumza na waandishi wa habari msiba wa Qaresi upo nyumbani kwake Salasala, Dar es Salaam. Mwili wake utaagwa rasmi siku ya Jumamosi, tarehe 12 Julai 2025, na baada ya hapo atasafirishwa kuelekea nyumbani kwao Manyara kwa ajili ya maziko yatakayofanyika Jumatatu, tarehe 14 Julai 2025.
Mateo T. Qaresi alihudumu kama Mbunge wa Babati kuanzia mwaka 1985 hadi 2000, kipindi ambacho alishika nyadhifa mbalimbali za juu serikalini. Alikuwa Waziri wa Ushirika na Masoko kati ya mwaka 1989–1994, Waziri wa Utumishi wa Umma kati ya mwaka 1995–1997, na baadaye Waziri wa Masuala ya Nchi – Ofisi ya Rais kati ya 1997–2000.
Mwaka 2001, Qaresi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, nafasi aliyoitumikia hadi alipostaafu mwaka 2006.
Qaresi atakumbukwa pia kama mmoja wa wanachama mashuhuri wa kundi la G55, kundi la wabunge 55 waliokuwa mstari wa mbele mwaka 1993 kupaza sauti kuhusu utata wa muundo wa Muungano wa Tanzania. G55, lililoongozwa na Njelu Kasaka na kuhusisha majina makubwa katika siasa za Tanzania kama Generali Ulimwengu na Balozi George Maige Nhigula lilipendekeza kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya mfumo wa serikali tatu: Muungano, Zanzibar na Tanganyika. Ingawa hoja hiyo haikufanikiwa baada ya Mwalimu Julius Nyerere kuingilia kati, ilibaki kuwa sehemu ya historia ya harakati za mageuzi ndani ya Bunge.
Qaresi atakumbukwa kwa misimamo yake thabiti, uzalendo na ujasiri wa kisiasa uliomweka katika safu ya viongozi waliogusa maisha ya Watanzania wengi kupitia sera na utumishi uliotukuka.