Dodoma Watu wanne wamepoteza maisha huku wengine 18 wakijeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta wa kanisa wakati wa ibada ya ubatizo iliyofanyika Desemba 23 mwaka huu katika Parishi ya Wiliko Dinari ya Mpwayungu wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Akizungumza kuhusu tukio hilo jana Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk. Dickson Chilongani alisema kuwa miongoni mwa waliopoteza maisha ni mke wa Kasisi wa Dinari ya Mpunguzi, Dina Machela.
Askofu Chilongani alisema kuwa wakati wa tukio hilo kulikuwa na ibada ya ubatizo katika kanisa hilo lakini kabla ya ibada kuhitimishwa dalili za mvua zilianza kuonekana.
“Kutokana na hali hiyo ya hewa, mchungaji alihitimisha ibada mapema ili waumini waweze kutawanyika. Baadhi yao walifanikiwa kurejea majumbani, huku wengine wakiamua kubaki kanisani kujikinga na mvua,” alisema.
Aliongeza kuwa mvua ilianza kunyesha ikifuatana na upepo mkali hali iliyosababisha ukuta mmoja wa kanisa hilo kuanguka, na kuua watu wawili papo hapo pamoja na kuwajeruhi wengine 18.
Aidha Askofu Chilongani alisema kuwa watu wengine wawili akiwamo mke wa kasisi walifariki dunia wakiwa njiani wakikimbizwa katika vituo vya afya kwa ajili ya kupata matibabu.
Tukio hilo limeacha majonzi makubwa kwa waumini na wakazi wa eneo hilo huku mamlaka husika zikiendelea kufuatilia chanzo cha kuanguka kwa ukuta huo na hali za majeruhi waliolazwa hospitalini.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime