Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) inaendelea kushika kasi nchini Morocco, huku mashindano hayo yakizidi kuvutia mashabiki wa soka barani Afrika.
Usiku wa kuamkia leo, timu ya taifa ya Cameroon iliibuka na ushindi mwembamba wa bao 1–0 dhidi ya Gabon katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa. Ushindi huo umeipa Cameroon mwanzo mzuri katika kampeni yao ya michuano hiyo.
Katika michezo ya jana Jumatano, Algeria ilionesha ubabe kwa kuicharaza Sudan kwa mabao 3–0, huku mabingwa watetezi Ivory Coast wakipata ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Msumbiji katika mchezo uliokuwa na presha kubwa.
Matokeo hayo yamehitimisha rasmi mzunguko wa kwanza wa hatua ya makundi kwa kila timu, na sasa macho na masikio yanaelekezwa kwenye mechi za mzunguko wa pili zinazotarajiwa kuanza kesho.
Ratiba ya kesho inaonesha Misri wakianza mapema dhidi ya Afrika Kusini, ikifuatiwa na Zambia watakaovaana na Comoro, huku mechi ya usiku ikiwakutanisha wenyeji Morocco dhidi ya Mali katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Mashabiki wanatarajia kuona matokeo yatakayochanganya zaidi msimamo wa makundi na kuanza kutoa taswira ya timu zitakazofuzu hatua ya mtoano.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime