Watu watano wamepoteza maisha kufuatia ajali ya helikopta iliyoanguka katika Mlima Kilimanjaro,mlima mrefu zaidi barani Afrika katika tukio lililotokea Jumatano jioni wakati wa operesheni ya uokoaji.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi helikopta hiyo ilikuwa ikifanya operesheni ya kuchukua wagonjwa waliokuwa wakipanda mlima huo kupitia moja ya njia maarufu za kupandia.
Wawili kati ya waliokufa walikuwa wageni waliokuwa wameokolewa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Ajali hiyo pia ilisababisha vifo vya daktari wa ndani mwongozaji wa watalii pamoja na rubani wa helikopta hiyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro Simon Maigwa, alisema helikopta hiyo ilikuwa mali ya kampuni ya Kilimanjaro Aviation inayojihusisha na huduma za uokoaji wa wagonjwa usafiri wa anga na shughuli nyingine za anga katika eneo la mlima huo.
Taarifa zinaeleza kuwa helikopta ilianguka kati ya Kambi ya Barafu na Kilele cha Kibo katika kimo cha zaidi ya mita 4,000 juu ya usawa wa bahari eneo linalojulikana kuwa na hali ngumu ya kijiografia na mabadiliko ya ghafla ya hali ya hewa.
Polisi wamesema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo huku wakiahidi kutoa taarifa zaidi kadri uchunguzi utakavyokuwa unaendelea.
Ajali za anga katika Mlima Kilimanjaro ni nadra kutokea ambapo yukio la mwisho la aina hiyo liliripotiwa mwezi Novemba mwaka 2008 ambapo watu wanne walipoteza maisha.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime