Chama cha ACT-Wazalendo kimesisitiza kuwa ni marufuku kwa wanachama na wafuasi wake kufurahia uovu wowote unaofanywa na vyombo vya dola bila kujali mhanga ni nani, ikiwemo wanachama wa vyama pinzani au chama tawala.
Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema dhamira ya chama hicho ni kupambana na dhuluma yoyote inayofanywa na dola, bila kujali chama, dini au itikadi ya mhusika.
Akitolea mfano wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Ado alisema licha ya kwamba askofu wake ni kada wa CCM na chama hicho kuwa na misimamo inayotofautiana na ACT, bado walipaza sauti dhidi ya kufungiwa kwake, kwa sababu kilichofanyika ni uonevu.
Amesema watu wanaopanga kufanya mashambulizi katika ibada za Jumapili maeneo kama Ubungo ni maadui wa taifa na wanacheza na jambo nyeti linaloweza kusababisha maafa makubwa kitaifa.
Vilevile, Ado ametoa wito wa kutofurahia dhuluma dhidi ya vyama vingine vya upinzani, akisisitiza kuwa ACT-Wazalendo imekuwa mstari wa mbele kupinga kushikiliwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu kwa kile alichokiita kesi ya kisiasa.
Kauli hiyo ya Ado inaonekana kuwa mwitikio wa matukio ya hivi karibuni ya ukiukwaji wa haki za kidemokrasia nchini na inalenga kutoa msimamo wa chama hicho kuhusu umuhimu wa kutetea haki na amani kwa kila Mtanzania bila ubaguzi.