Ombi la Chadema kumkataa jaji kusikilizwa leo Mahakama kuu

Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam leo  Julai 14 mwaka huu inatarajia kusikiliza maombi ya Chadema ya kumtaka Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama hicho, kujiondoa kwenye kesi hiyo.

Maombi hayo yanatarajiwa kusikilizwa wakati kesi ya msingi ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Julai 10 mwaka huu hama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Bodi ya Wadhamini wake waliosajiliwa kiliwasilisha maombi rasmi ya kumtaka Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi yake ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama, ajiondoe kwenye kesi hiyo.

Pia chama hicho kilifungua shauri la maombi kikiiomba Mahakama hiyo iondoe amri zake za zuio dhidi ya wadaiwa katika kesi hiyo (Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu), kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama.

Siku hiyo wakati kesi ya msingi ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji kiongozi wa jopo la mawakili wa wadaiwa Mpale Mpoki aliieleza Mahakama kuwa wadaiwa hao (bodi ya wadhamini na katibu mkuu) wameandika barua ya kumtaka jaji huyo ajitoe katika kesi hiyo.

Wakili Mpoki alidai barua hiyo iliyoandikwa Juni 23 mwaka huu iliwasilishwa kwa Naibu Msajili Juni 24 mwaka huu. 

Kwa upande wake, wakili wa wadai, Shabani Marijani alidai walipata taarifa za kuwepo kwa barua hiyo ya wadaiwa kumkataa jaji siku hiyo asubuhi.

Hivyo walidai kwa kuwa suala la kumkataa jaji ni la kisheria, wanaomba ahirisho la muda wa kuipitia ili kuona kama kuna hoja huku akiiomba Mahakama iwape muda mfupi kwa kuwa shauri hilo linagusa masilahi ya umma.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii