Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma imeondoa shauri la awali lililofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church (Ufufuo na Uzima), linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima kufuatia hatua ya Serikali kulifungia kanisa hilo.
Maombi ya kuondoa shauri hilo yaliwasilishwa na Wakili Alphonce Nachipyangu, baada ya Serikali kuwasilisha barua rasmi inayomtaja mteja wao kwa jina sahihi linalotambulika kisheria, hivyo wanasheria wa kanisa hilo wanatarajia kuwasilisha maombi mapya kwa kufuata taratibu zote.
Aidha Juni 2 mwaka huu waumini wa kanisa hilo walizuiwa kufanya ibada baada ya Vyombo vya Dola kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya Kanisa hilo. Ikumbukwe pia, waumini 52 walifungua kesi dhidi ya Mwanasheria Mkuu na Mkuu wa Jeshi la Polisi wakidai kukamatwa na Polisi Juni 29mwaka huu wakiwa katika ibada eneo la Ubungo, wakitekeleza haki yao ya kikatiba ya kuabudu.