Vuguvugu laibuka CCM kufuatia tuhuma za kupokea rushwa dhidi ya Ibrahim Mzava.

Mchakato wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuwapata wagombea wa ubunge na udiwani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 umeelezwa kuingia katika hali ya sintofahamu kufuatia tuhuma nzito dhidi ya Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Ibrahim Mzava.

Mzava anatuhumiwa na wanachama wenzake kuendesha mchakato huo kwa misingi ya ubaguzi wa kidini na pia kuomba fedha kutoka kwa baadhi ya watia nia wa ubunge katika Jimbo la Mwanga.

Sauti inayodaiwa kuwa ya Mzava imevuja na kusambaa mitandaoni, ikimuonesha akizungumza na mmoja wa watia nia huku wakisisitiza umuhimu wa nafasi ya ubunge kushikiliwa na mtu kutoka dini ya Kiislamu.

Katika sauti hiyo, mtu anayedaiwa kuwa mwenyekiti huyo anasikika akisema: "Tutakuja ulizwa siku ya kiama, tutaulizwa. Hivyo tuhakikishe tunatafuta Muislamu safi wa kukaa hapo kwenye kiti."

Mbali na kauli hiyo, kuna kauli inayodaiwa kumhusisha Mzava akizungumza na mtia nia mwingine kuhusu mahitaji ya fedha, hali iliyozua tuhuma za kuomba au kupokea rushwa.

"Wewe nitumie tu kwenye namba hii…tena nilikuwa na hali ngumu sana jina Ibrahim Mzava…Kuna mahali fulani tunakwenda na Sheikh nilikuwa ninakutafuta ili utusaidie mafuta…tulikuwa na vikao vya kata, Sheikh alikuwa alikuwa anakwenda kuonana na Wajumbe Mkutano Mkuu wa kila kata, sasa tulikuwa tunahangaika mafuta, nimekupigia tangu juzi…”, alisikika akiongea anayeelezwa kuwa Mzava baada ya anayeongea naye (mtia nia) kumwambia kuwa angemtumia Shilingi laki moja na nusu au mbili.

Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa ya Julai 15 mwaka huu Mzava alikana kuhusika moja kwa moja na sauti hiyo alipopigiwa simu akisema: “Mimi si Mkurugenzi wa Uchaguzi. Hayo masuala aulizwe Mkurugenzi wa Uchaguzi”, kisha akakata simu na hakupatikana tena kwa mawasiliano ya ziada.

Wakuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wameendelea na uchunguzi kuhusu tuhuma mbalimbali zilizowasilishwa na wagombea, wajumbe na wafuasi katika mchakato wa kura za maoni sehemu mbalimbali, wakieleza kuwa macho hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii