Tasnia ya filamu ya India imegubikwa na simanzi kufuatia kifo cha mmoja wa nguli wake wakubwa na kipenzi cha vizazi vingi Dharmendra Kewal Krishan Deol ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 89
Baada ya taarifa za msiba kutangazwa, mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vilijaa salamu za rambirambi, huku mastaa wa Bollywood wakimiminika kutoa heshima zao za mwisho, kumkumbuka kama gwiji aliyeibadilisha sekta ya filamu na kuacha alama isiyofutika.
Miongoni mwa walioongoza kutoa salamu za rambirambi ni Karan Johar, ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika kuwa Dharmendra alikuwa “mwalimu, gwiji na msaada mkubwa kwa kizazi kipya cha wasanii”. Naye Ajay Devgn alieleza masikitiko yake akimuelezea marehemu kama “msanii aliyeunganisha vizazi na kuifanya Bollywood ijulikane kimataifa.”
Kajol, akitoa salam zake, alisema Dharmendra alikuwa mfano wa kuigwa kwa unyenyekevu, ubunifu na moyo wa kusaidia wengine, akisisitiza kuwa mchango wake katika tasnia utaendelea kuishi milele kupitia kazi zake.
Dharmendra ameacha mjane na watoto sita ambao ni Sunny Deol, Bobby Deol, Vijeta na Ajeeta (na Prakash Kaur), pamoja na Esha Deol na Ahana Deol (na Hema Malini).
Aidha Dharmendra aliigiza zaidi ya filamu 250, alijulikana kwa mvuto wake wa kipekee, umahiri wa uigizaji na uwezo wa kucheza aina mbalimbali za majukumu, kuanzia drama na filamu za mapigano, umaarufu wake ulimpa nafasi ya kuwa miongoni mwa nguli wa filamu za India waliounganisha tamaduni na vizazi tofauti.
Na@MustaphaKinkulah
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime