Kamishna wa Masuala ya Kibinadamu wa Ulaya kuzuru Bunia nchini

Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa, Misaada ya Kibinadamu na Mwitikio wa Migogoro wa Ulaya, Hadja Lahbib, anatarajiwa Jumapili hii, Juni 7, kwa ziara fupi Bunia mashariki mwa DRC. Mji mkuu wa mkoa wa Ituri umekuwa ukikabiliwa na mlipuko mpya wa Ebola tangu Mei 15.

Umoja wa Ulaya umejitolea kukabiliana na janga la Ebola. Umetenga euro milioni 15 za ziada kama msaada wa kibinadamu kwa DRC, na pia kwa Uganda, nchi nyingine ambayo kwa sasa inakabiliwa na kuibuka tena kwa ugonjwa huo. EU pia imeanzisha usafiri wa anga ambapo ilipeleka karibu tani 100 za vifaa huko Bunia katika siku za hivi karibuni.

Kwa jumla, ndege nane zilikodishwa na shirika la kibinadamu la Umoja wa Ulaya, ECHO, na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, kusafirisha vifaa muhimu hadi Ituri kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo. Zilitua Bunia katika siku za hivi karibuni, baada ya kusafiri kutoka Nairobi, Kenya. Safari hii ya ndege ilitamatika siku ya Ijumaa kwa shehena mbili za mwisho.

Tani hizi 100 za vifaa zilisambazwa miongoni mwa wahusika mbalimbali huko Bunia. Usafirishaji huo ulijumuisha mahema, dawa, na vifaa vya kinga. Pia waliunga mkono kuanzishwa kwa vituo kadhaa vya matibabu ya Ebola karibu na Bunia, kitovu cha mlipuko huo. Kamishna wa Ulaya anatarajiwa kuzuru vituo hivi leo Jumapili Juni 7.

Hadja Lahbib pia atakutana na viongozi mbalimbali huko Bunia, akiwemo gavana mpya wa kijeshi wa mkoa huo, Meja Jenerali Gaby Kasongo Mulumba, aliyeteuliwa siku ya Ijumaa kuchukua nafasi ya Jenerali Johnny Luboya.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii