WATU wanaoshukiwa kutumia TikTok kuwavuta vijana katika mitego ya uhalifu wamekamatwa na polisi jijini Nairobi, huku uchunguzi ukionyesha huenda kuna wahalifu wanaowalenga Wakenya mitandaoni.
Washukiwa hao, Emanuel Bosire Arisa, Brian Gatheru Nderitu na mtoto mmoja, wanazuiliwa kwa siku 21 huku wapelelezi wakikusanya ushahidi dhidi yao.
Kwa mujibu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), washukiwa hao walikuwa wakiendesha ukurasa wa TikTok usiojulikana walioutumia kuwasiliana na waathiriwa kabla ya kupanga kukutana nao ana kwa ana.
Mmoja wa waathiriwa ni Nzumari, jina limebadilishwa kwa sababu ni mtoto, ambaye alikutana na washukiwa hao baada ya kwanza kumsifu kupitia TikTok na baadaye kumshawishi kuhamishia mazungumzo WhatsApp.
Mazungumzo hayo yaligeuka kuwa ya kimapenzi kabla ya washukiwa kumwalika Ruai, Nairobi, akiamini angeenda kujiburudisha.
Hata hivyo, inadaiwa walimpeleka eneo lililotengwa ambako walimnyanyasa kingono na kumpora simu.
Washukiwa hao pia walidaiwa kumlazimisha kutoa nambari yake ya siri ya M-Pesa.
Baadaye walimtishia mama yake wakimtaka atume pesa zaidi na kumuonya kuwa wangemtupa Nzumari iwapo hangetii.
Hatimaye walimwacha katika eneo asilolijua akiwa amesononeka.
DCI ilisema washukiwa hao wametambuliwa na waathiriwa watano katika visa tofauti vilivyoripotiwa Buruburu, Embakasi na Ruai.
Afisa wa DCI wa Ruai Henry Kinyua alisema polisi wamepokea visa sita vyenye mtindo unaofanana huko Ruai tangu Julai. Kisa kingine kiliripotiwa Imara Daima na viwili Buruburu.
“Baada ya anayelengwa kuwaamini, mtu huyo humwaalika walale kwake au kwenda kujiburudisha. Lakini mwaathiriwa anapofika, hugeukwa kisha huibiwa na hata kudhulimiwa kimapenzi,” akasema Bw Kinyua.
Polisi walipata simu sita kutoka kwa washukiwa hao pamoja na makoti mawili yenye kofia yaliyodaiwa kutumiwa kuficha utambulisho wao wakati wa uhalifu.
Bw Kinyua alisema mmoja wa washukiwa alikuwa akimtumia mdogo wake kuwachukua waathiriwa, kwa kuwa umri wake uliwafanya wasiwe na mashaka.
Alisema washukiwa hao pia walitumia picha na video zinazoonyesha maisha ya kifahari kwenye mitandao kuwavutia waathiriwa.
“Tulipofungua kurasa hizo tuligundua kuwa kijana huyo anachapisha sana maisha ya kifahari, hali iliyowavutia watu kwa mtu huyu anayeishi maisha ya kifahari ilhali kumbe ni mhalifu,” akasema.
Mwanasaikolojia wa watoto na vijana Winnie Ndung’u alisema vijana wako katika hatari ya kutumiwa na wanyanyasaji kwa sababu akili zao bado zinaendelea kukomaa.
“Wanatumia ukweli kwamba akili ya mtoto bado haijakomaa kikamilifu ili kufanya maamuzi thabiti na huanza kuwavutia kwa mambo wanayopenda kabla ya kuwanyanyasa,” akasema.
Ripoti ya UNICEF ilionyehsa kuwa asilimia 67.3 ya watoto walipitia unyanyasaji.
Kati yao, asilimia 25.5 hawakujua mahali pa kuripoti, asilimia 22.1 waliona aibu, huku asilimia 14.6 wakiogopa kupata matatizo iwapo wangezungumza.