Prof. Shemdoe azitaka wilaya, halmashari zote kujiandaa kukabiliana na athari za mvua za El nino

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amezielekeza Wilaya na Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinafanya kazi ya kuzibua mitaro na mifereji ya maji ili kujiandaa na kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi Oktoba 2026 hadi Februari 2027, kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo Septemba 13, 2026 akiwa Somanga, wilaya ya Kilwa, katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi mkoani Lindi, yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuhimiza uwajibikaji kwa viongozi na watumishi wa umma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Prof. Shemdoe amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Mameneja wa TARURA Wilaya nchini kote, kuhakikisha wanashirikiana na taasisi nyingine katika kujiandaa na kuwa na utayari wa kukabiliana na athari za mvua za El Niño kwa kuhakikisha miundombinu ya kupitisha maji inakuwa katika hali nzuri na inakidhi mahitaji.

“Nimuelekeze Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kushirikiana na wananchi kuzibua mifereji ya maji iliyoziba ili kipindi cha mvua za El Niño maji yasipate nafasi ya kuchepuka na kuvamia makazi ya wananchi na kuleta madhara, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa simamia jambo hili,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Katika hatua nyingine, akijibu ombi la wananchi wa kata ya Kinjumbi la kujengewa kwa kiwango cha lami

barabara ya Kinjumbi yenye urefu wa kilomita 30, Prof. Shemdoe amesema ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami utachukua muda mrefu, hivyo amemuelekeza Meneja wa TARURA kufanya tathmini ya gharama za kuikarabati kwa kiwango cha changarawe na kuwasilisha gharama hizo ofisini kwake ili bajeti ya fedha za matengenezo itumike kuikarabati na kuiwezesha kutumika muda wote.

Maelekezo ya Prof. Shemdoe kwa wilaya na halmashauri kujiandaa kukabiliana na athari za mvua za El Niño ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa katika kikao kazi Septemba 11, 2026 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, aliyezitaka Wizara, Mamlaka na Taasisi zinazohusika kuchukua hatua za haraka za kujiandaa ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba 2026.

Aidha, maelekezo hayo ya Prof. Shemdoe kwa wilaya na halmashauri kujiandaa kukabiliana na athari za mvua za El Niño ni muendelezo wa hatua za utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha usafi wa mazingira katika miji na majiji, aliyoyatoa Septemba 2, 2026 wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala aliowateua Agosti 27, 2026.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Somanga, mkazi wa kata ya Somanga, wilaya ya Kilwa, Bw. Hashimu Omary Changadua, ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea shule mbili za sekondari, soko la kimkakati na kituo cha afya, pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Mara baada ya kuzungumza na wananchi wa Somanga, Prof. Shemdoe aliendelea na ziara yake kwa kutembelea na kukagua ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao linalojengwa na halmashauri ya Kilwa, pamoja na ujenzi wa soko la wajasiriamali wadogo katika kijiji cha Njianne, kata ya Tingi, katika halmashauri hiyo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii