Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imemhukumu kifo aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila baada ya kumtia hatiani kwa makosa kadhaa makubwa yakiwemo uhaini, uasi na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Hukumu hiyo imetolewa jana Jumanne na Luteni Jenerali Joseph Mutombo Katalayi mjini Kinshasa bila ya yeye mwenyewe kuwepo.
Kabila alipatikana na hatia ya kushirikiana na kundi la waasi la M23 linaloipinga serikali, na ambalo limeteka maeneo mengi ya mashariki mwa Kongo yenye utajiri mkubwa wa rasilimali wakisaidiwa na Rwanda.
Aliondoka nchini humo mwaka 2023 na kuonekana tena mwezi Mei mwaka huu katika mji wa Goma unaokaliwa na waasi hao hatua iliyoibua wasiwasi mjini Kinshasa.
Wafuatiliaji wa mambo wanasema hukumu hiyo inalenga tu kuzuia azma yake ya kuunganisha upinzani, licha ya kwamba hajulikani aliko kwa sasa.