Mwakinyo Arejea Kileleni Afrika, Ashika Nafasi ya 37 Duniani (Middleweight)

Bondia wa kulipwa kutoka nchini Tanzania Hassan Mwakinyo Jr ametangaza kurejea nafasi ya kwanza barani Afrika katika uzito wa kati (middleweight) na kushika nafasi ya 37 duniani kati ya mabondia 1,950, kwa mujibu wa viwango vipya vya ubora duniani vya Boxing Record.

Mwakinyo ametoa taarifa hiyo kupitia ujumbe aliouandika kwenye mitandao ya kijamii, akieleza kuwa ushindi wake wa hivi karibuni dhidi ya bondia aliyemuita “mlemvi” na asiye kuwa kiwango chake, ndio uliomrejesha kwenye nafasi yake ya juu barani Afrika.

Katika ujumbe huo Mwakinyo amesema mafanikio hayo yamemrudisha kwenye heshima yake na kutuma ujumbe kwa wanaopotosha tasnia ya masumbwi.

Ameeleza kuwa licha ya kutokuwa na ulazima wa kujisifia ameona ni vyema kuweka wazi mafanikio yake kutokana na kuwepo kwa mabondia na wadau wanaotoa taarifa zisizo sahihi.

Hata hivyo Mwakinyo amehitimisha kwa kusisitiza kuwa yupo tayari kukabiliana na changamoto zozote akisema, “Mapovu ruksa,” kauli inayoashiria kujiamini na dhamira yake ya kuendelea kutawala katika masumbwi ya Afrika na dunia.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii