Ushiriki wa timu ya taifa ya Eritrea katika michuano ya awali kufuzu kucheza fainali za kombe la mataifa ya Afrika, sasa umeleta maswali zaidi baada ya wachezaji wake 7 kuzamia nchini Eswatini baada ya ushindi uliofanikisha wafuzu hatua ya makundi kusaka tiketi ya AFCON 2027.
Wachezaji hao walitoweka baada ya Eritrea kupata ushindi wa jumla ya mabao manne dhidi ya Eswatini Machi 31, tukio hili likiwa ni muendelezo wa mtindo ambao umebainisha ushiriki wao wa kimataifa katika miongo miwili iliyopita na kusababisha Eritrea kushiriki mara chache katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa ya Afrika.
Ushindi dhidi ya Eswatini ulithibitisha mafanikio ya kushangaza kwa Eritrea yenye nafasi ya chini kwenye soka ikizingatiwa kuwa hawakuwa wamecheza mechi ya kimataifa kwa miaka sita.
Hii si mara ya kwanza kwa wachezaji wa Eritrea kuomba hifadhi katika nchi wanakoenda kucheza, ambapo baadhi walifanya hivyo mwaka 2007 huko Angola, Kenya mwaka 2009, Tanzania mwaka 2011, Botswana mwaka 2015, Uganda mwaka 2012 na 2019.
Inakadiriwa kuwa takriban wachezaji 80 wa mpira wa miguu wamekimbia nchi yao wakati wakiichezea timu ya taifa, huku kukiwa hakuna hata mmoja wao anayeendelea kucheza soka uhamishoni.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu, yanautuhumu utawala wa rais Isaias Afwerk, kutekeleza vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu, tangu ilipopata uhuru toka kwa Ethiopia mwaka 1993.