SERIKALI imesema usimamizi wa taka hususan katika maeneo ya mjini hauridhishi, kwa kuwa ni wastani wa asilimia 37 tu ya taka ngumu zinazozalishwa, ndizo hukusanywa, hivyo kiasi kikubwa kinachosalia huzagaa.
Hata hivyo, wito umetolewa kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo ya kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, unafanyika.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Yussuf Masauni ameyasema hayo mara baada ya kuongoza kufanya usafi katika Soko la Buguruni, jijini Dar es Salaam, jana Septemba 5, 2026.
“Tunakumbuka kuwa serikali kupitia Rais akiwa Makamu wa Rais mwaka 2016 alitoa agizo kuwa kila Jumamosi ya mwisho ya mwezi kuwa siku ya usafi wa Mazingira Kitaifa.”
Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa ‘Enviromental Management (Designation of National Cleanliness Day) Guidelines , 2016,chini ya G.N.No.139. Mwongozo huo unaelekeza utekelezaji wa tamko la Serikali la kuitangaza kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuwa siku ya usafi wa Mazingira Kitaifa.
“Kwa muktadha huo, Serikali inatoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kuhakikisha kuwa wanaweka utaratibu wa kusimamia utekelezaji wa maelekezo haya kwa kuzingatia maslahi ya makundi mbalimbali.
“Ni wajibu wa kila mwananchi, mfanyabiashara, mwekezaji, taasisi za serikali, sekta binafsi, viongozi wa mitaa, wenye viwanda, watoa huduma za taka, taasisi za elimu na jamii kwa ujumla kuwa na utaratibu wa kufanya na kusimamia usafi wa mazingira katika maeneo yao.
Hivyo serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamtaka kila Mtanzania kushiriki katika usafi wa mazingira,” alisema Masauni.
Amesema, taka zinapotupwa hovyo, mifereji inapoziba, maeneo ya biasharayanapokuwa machafu au taka ngumu na hatarishi zinaposhughulikiwa bila utaratibu, madhara yake huonekana katika afya ya wananchi, miundombinu, mito, bahari na uchumi.
Masauni amesema mazingira machafu yanaweza kuchangia kuenea kwa magonjwa, kuongeza gharama za usafi na afya, kupunguza mvuto wa miji yetu kwa watalii na wawekezaji na kuharibu rasilimali ambazo Watanzania wanategemea kwa maisha yao.
Amesema, taka zinaweza kuwa fursa ya kiuchumi kupitia urejelezaji uchumi rejeshi, taka kutumika kama chanzo cha uzalishaji wa nishati, uzalishaji wa mbolea (mboji) na biashara ya kaboni.
Tanzania ina fursa ya uwekezaji wenye thamani ya takribani Sh. bilioni 22 kutoka katika taka plastiki, karatasi chakavu, taka za kielektroniki na betri chakavu.